Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لآيَاتٍ لِّأُوْلِي الألْبَابِ)) ((الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىَ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّار))
((Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili)) ((Ambao humkumbuka Allaah wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto)) [Al-'Imraan: 190-191]
Aayah hizo mbili tukufu ni Aayah ambazo zinaonyesha dalili ya Tawhiyd kwa watu wanaofahamu, watu wanaotafakari ambao wanadhihirisha imani zao kutokana kuonekana tabia zao, usemi wao,na kumkumbuka Mola wao kwa du'aa na adkhaar kila wakati na popote walipo.
Na hakika mwenye kutafakari maumbile ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), ndio waliokusudiwa kuwa ni 'Ulil-Al-Baab' (Wenye akili). Nao hukaa na kutafakari mbingu na ukubwa wake, umbali wake, ulimwengu mzima ulivyo mkubwa na mpana, uzito, na viliomo ndani yake vya ajabu, nyota mbali mbali zinazozunguka angani, bahari, milima, mabonde, chemchemu za maji, mito, majangwa, miti, mimea, maua yenye rangi na harufu mbali mbali, matunda ya kila aina kwa rangi na ladha mbali mbali ambayo yote yanatokana na maji (mvua) hiyo hiyo aina moja tu, wanyama, madini, na mengi mengine ambayo hayahesabiki. Wenye akili hutafakari pia kuhusu nafsi zao, mwili wao ulivyoumbwa na kuwaza sababu ya kuumbwa vyote hivyo.
Juu ya hivyo kutafakari kwa kukhitilafiana wakati pia, mfano siku za majira ya baridi kuwa fupi na siku za majira ya joto kuwa refu, kugeuka mchana, usiku na kupambazuka kwa Alfajiri, yote hayo ni kwa amri na uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Mwenye Hikma zote daima na ndio maana Anasema:
(( لآيَاتٍ لِّأُوْلِي الألْبَابِ))
((bila shaka ni Ishara kwa wenye akili))
Wanakusudiwa hapa walio werevu wenye mawazo ya kutafakari sana kuhusu ukweli wa mambo ya maumbile ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na sio waliokuwa kama vipofu wasiokuwa na mawazo kabisa ya kufikiri maumbile ya Mola wao wanayoishi nayo kila siku, yanayoonekana kila mahali walipo mchana na usiku, na hata kama wanajua kuwa ni maumbile ya Muumba Mwenye Nguvu na Uwezo wote, lakini hawana hamu ya kumtambua na kumuamini, bali wanapuuza. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anataja kupuuza kwao haki hii :
(( وَكَأَيِّن مِّن آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ)) ((وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُمْ بِاللّهِ إِلاَّ وَهُم مُّشْرِكُونَ))
((Na ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazozipitia, na hali ya kuwa wanazipuuza)) ((Na wengi katika wao hawamuamini Allaah pasina kuwa ni washirikina)) [Yuusuf:105-106]
Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kawaelezea wale wenye kutafakari kuwa wao wanamkumbuka Mola wao kila wakati, popote walipo, vyovyote walivyo na wanashuhudia Utukufu, Uwezo, Ujuzi, Hikma na Rehma ya Muumba wao, kisha humtukuza Mola wao na kutambua kwa kukiri kuwa hakika Hakuviumba vyote hivyo bila ya sababu bali Kaviumba kwa haki ili awalipe wanaotenda maovu adhabu wanazostahiki na Awalipe wanaofanya mema Pepo wanayostahiki. Na kwa kumalizia humuomba Mola wao Awaepushe na adhabu ya moto.
((الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىَ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّار))
((Ambao humkumbuka Allaah wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu!! Hukuviumba hivi bure. Subhaanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto)) [Al-'Imraan:191]
Hali ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilivyokuwa wakati zimeteremshwa Aayah hizi:
روي أن عائشة أم المؤمنين رضي الله عنها سئلت عن أعجب ما رأته من رسول الله صلى الله عليه وسلم فبكت ثم قالت: كان كل أمره عجباً، أتاني في ليلتي التي يكون فيها عندي، فاضطجع بجنبي حتى مس جلدي جلده، ثم قال: ((ياعائشة ألا تأذنين لي أن أتعبد ربي عز وجل؟)) فقلت: يارسول الله: والله إني لأحب قربك وأحب هواك- أي أحب ألاّ تفارقني وأحب مايسرك مما تهواه- قالت: فقام إلى قربة من ماء في البيت فتوضأ ولم يكثر صب الماء، ثم قام يصلي ويتهجد فبكى في صلاته حتى بل لحيته، ثم سجد فبكى حتى بلّ الأرض، ثم اضطجع على جنبه فبكى، حتى إذا أتى بلال يؤذنه بصلاة الفجر، رآه يبكي فقال يارسول الله: مايبكيك وقد غفر الله لك ماتقدم من ذنبك وماتأخر؟ فقال له: ((ويحك يابلال، ومايمنعني أن أبكي وقد أنزل الله عليّ في هذه الليلة هذه الآيات : (إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لآيَاتٍ لِّأُوْلِي الألْبَابِ... ) ثم قال: ((ويل لمن قرأها ولم يتفكر فيها)).
Imesimuliwa kwamba Mama wa Waumini 'Aishah (Radhiya Allahu 'anhaa) aliulizwa kuhusu jambo la ajabu alilolishuhudia kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alilia kwanza kisha akasema: "Mambo yake yote yalikuwa ya ajabu. Usiku mmoja alikuja karibu na mimi mpaka ngozi yake ikagusa ngozi yangu na akasema, ((Huniaachi nimuabudu Mola wangu?)) Nikasema: "Ee Mjumbe wa Allaah, WaLLaahi, hakika mimi napenda ukaribu wako kwangu (uwe karibu yangu), na pia napenda mahaba yako, kwamba napenda usiwe mbali na mimi, na napenda yale yanayokufurahisha". Akasema ('Aishah): "Akainuka na kutumia kiroba cha maji na akafanya wudhuu wala hakutumia maji mengi. Kisha akasimama akaswali 'Tahajjud' akalia mpaka ndevu zake zikawa zimerowa. Kisha akasujudu na kulia mpaka akaifanya ardhi irowe. Kisha akalala kwa upande wa kulia mpaka akaja Bilaal kumjulisha Adhaan ya Alfajiri, akamuuliza: "Ee Mjumbe wa Allaah! Jambo gani linakuliza na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amekwishakufutia madhambi yako yaliyotangulia na yanayokuja?" Akasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ee Bilaal, na nini kinizuie mimi kulia wakati usiku huu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameniteremshia Aayah hizi?"
(( إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لآيَاتٍ لِّأُوْلِي الألْبَابِ ...))
((Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili)) ... (mpaka mwisho wa Surah hii ya Al-'Imraan)
Kisha akasema: ((Ole wake, yule anayezisoma lakini hatafakari kwayo))
Unapoamka Tahajjud ni Sunnah kuzisoma Aayah hizo kwani ilikuwa ni ada ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzisoma Aayah hizi anapoamka kuswali Tahajjud. Na sisi tunapaswa tufuate Sunnah hii tukufu.
Ndugu Waislamu, hizo ndizo Aayah ambazo zilimliza Mtume wetu mpenzi (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawa hakuweza kulala usiku huo akawa anazisoma na huku analia tu. Hakika ni Aayah tukufu mno zinazosisimua mwili na kushitua nyoyo za wenye akili. Lakini si nyoyo za kila mtu!
Je, tutakuwa katika wale wanaomkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kila wakati na popote tulipo?
Je, tutafikiria Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) wa kuumba vyote vilivyo ulimwenguni na katika nafsi zetu pia na kufikiria Ufalme na Utukufu wake? Lau kama tutatafakari tunaposoma au kusikia Aayah hizi basi na sisi tutalia kwa khofu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), lakini labda nyoyo zetu zimekuwa ngumu, kwa hivyo inatupasa tumuombe Allaah Atupe Nuru ya Qur-aan katika nyoyo zetu itujaze imani na khofu ya Mola wetu. Aamiyn.
اللهم إنا نسألك قلباً خاشعا ولساناً ذاكرا وعلماً نافعاً وعملاً صالحاً.
Allaahuuma innaa nas-alauka qalban khaashi'an, wa lisaanan-dhaakiran, wa 'ilman-naafi'an, wa 'amalan-swaalihan.
(Ya Allaah, tunakuomba nyoyo zenye khofu, na ndimi zenye kukukumbuka, na elimu yenye manufaa na vitendo vyema). Aamiyn
********
0 comments:
Post a Comment