Mfano Wa Neno Zuri (La Tawhiyd) Ni Kama Mti Mzuri (Mtende) Na Faida Zake
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللّهُ مَثَلاً كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاء))
((تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا وَيَضْرِبُ اللّهُ الأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ))
((Hebu hukuona vipi Allaah Alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni))
((Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake. Na Allaah Huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka)) [Ibraahiym: 24 25]
((وَمَثلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَار))
(( يُثَبِّتُ اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ وَيُضِلُّ اللّهُ الظَّالِمِينَ وَيَفْعَلُ اللّهُ مَا يَشَاء))
((Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, uliong'olewa juu ya ardhi. Hauna imara))
((Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Allaah Hufanya Apendavyo)) [Ibraahiym: 26-27]
Aayah hizi tukufu zina mafunzo muhimu kwetu yanayohusu Tawhiyd, (Kumpwekesha Allaah bila kumshirikisha na chochote) kuthibitika kauli duniani na Aakhirah na pia kutuonyesha tofauti ya matunda yanayotokana baina ya maneno mawili haya; neno la tawhiyd kuwa matunda yake ni kheri tupu, na neno la kufru kuwa matunda yake ni mabaya hayana thamani wala faida yoyote bali ni shari tupu.
'Aliy bin Abiy Twalhah amesimulia kwamba 'Abdullaah bin 'Abbaas amesema kuhusu:
((كَلِمَةً طَيِّبَة))
((neno zuri))
ina maana ni kushuhudia: 'Laa ilaaha illa-Allaah' (Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah).
((كَشَجَرةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاء)) ((تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا))
((Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni))
((Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake))
'Abdullaah bin 'Abbaas amesema kuhusu ((Kama mti mzuri)) "ni mti wa Peponi" [At-Twabariy 16:573]
Ad-Dhwahaak, Sa'iyd bin Jubayr, 'Ikirimah, Mujaahid na wengineo wamesema, maana ya mfano huu wa huo mti mzuri unaotoa matunda yake kila mara, ni kama Muumini ambaye naye hufanya vitendo vyema kila mara usiku na mchana navyo vinapanda juu kila mara mchana na usiku. [At-Twabariy 16:572-573]
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutajia huo mti khaswa jina lake kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ اِبْن عُمَر قَالَ : كُنَّا عِنْد رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ ((أَخْبِرُونِي عَنْ شَجَرَة تُشْبِه - أَوْ - كَالرَّجُلِ الْمُسْلِم لَا يَتَحَاتّ وَرَقهَا صَيْفًا وَلَا شِتَاء وَتُؤْتِي أُكُلَهَا كُلّ حِين بِإِذْنِ رَبّهَا )) قَالَ اِبْن عُمَر : فَوَقَعَ فِي نَفْسِي أَنَّهَا النَّخْلَة وَرَأَيْت أَبَا بَكْر وَعُمَر لَا يَتَكَلَّمَانِ فَكَرِهْت أَنْ أَتَكَلَّمَ فَلَمَّا لَمْ يَقُولُوا شَيْئًا قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((هِيَ النَّخْلَة)) فَلَمَّا قُمْنَا قُلْت لِعُمَرَ : يَا أَبَتَاهُ وَاَللَّه لَقَدْ كَانَ وَقَعَ فِي نَفْسِي أَنَّهَا النَّخْلَة قَالَ مَا مَنَعَك أَنْ تَتَكَلَّم ؟ قُلْت لَمْ أَرَكُمْ تَتَكَلَّمُونَ فَكَرِهْت أَنْ أَتَكَلَّم أَوْ أَقُول شَيْئًا قَالَ عُمَر : لَأَنْ تَكُون قُلْتهَا أَحَبُّ إِلَيَّ مِنْ كَذَا وَكَذَا - البخاري
Kutoka kwa ibn 'Umar ambaye amesema: "Tulikuwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: ((Niambieni kuhusu mti unaofanana au kama Muislamu, ambao majani yake hayaanguki wakati wa majira ya joto wala wakati wa majira ya baridi na hutoa matunda yake kila mara kwa idhini ya Mola wake)) Ibn 'Umar akasema: "Niliufikiria kuwa ni mtende, lakini niliona haya kujibu nilipoona Abu Bakar na 'Umar hawakujibu. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ni mtende)). Tulipoondoka, nilimwambia 'Umar: Ewe baba yangu, WaLLaahi nilidhani kuwa ni mtende". Akasema: "Kwa nini basi hukutaja?" Nikasema: "Nilikuoneni kimya nikachukia (nikaona vibaya) kusema kitu". Akasema 'Umar: "Ungelisema ingelikuwa bora kwangu kuliko kadhaa na kadhaa" (Yaani ningelikuwa na fakhari zaidi kuwa wewe mwanangu ndiye uliyeweza kujibu pekee. [Al-Bukhaariy]
Hebu basi tutazame sifa za mti huu mzuri (mtende) na sifa za Muumimi tuone jinsi zilivyofanana:
Mtende:
Umethibiti ardhini kwa mizizi yake
Muumini:
Anathibiti Iymaan yake daima na huwa na Iymaan ya hali ya juu.
Mtende:
Tunda lake ni zuri na tamu.
Muumini:
Mazungumzo na vitendo vyake ni vizuri na vya kupendeza, na si mwenye maneno maovu yanayoudhi, kudharau, kukashifu, kusengenya, kufitinisha n.k.
Mtende:
Umepambika vizuri na kufunikika.
Muumini:
Mavazi yake ni mazuri ya heshima.
Mtende:
Ni wepesi kula tunda lake.
Muumini:
Ni wepesi kujadiliana na watu kwa hoja, dalili na kwa busara.
Mtende:
Una faida kwa anayekula, kwani matunda yake yana siha mwilini na huwa ni kinga ya maradhi, uchawi, na kila aina ya maovu kwa kula tende saba asubuhi kama kula chochote [Hadiyth kuhusu kula tende saba asubuhi katika Al-Bukhaariy na Muslim]
Muumini:
Iimu yake anayotoa ina faida kubwa ya kuwaongoza Waislamu na wasio Waislamu kutoka upotofu kuingia katika uongofu na hivyo ni kuutakasa moyo katika usalama wa shirki na maovu mengineyo, kinyume na moyo wenye maradhi ya shirki, unafiki n.k.
Mtende:
Ni mti madhubuti sana wenye kustahmili upepo mkali.
Muumini:
Iymaan yake imethibiti vizuri hata anapopata misukosuko na mitihani, huwa na moyo mkubwa wa kustahmili.
Mtende:
Kila unapokuwa mkubwa unazidi kutoa matunda na faida nyinginezo.
Muumini:
Kila anapozidi umri huongezeka elimu, busara na huzidi kunufaisha watu kwa kheri zake.
Na Allaah Anajua zaidi
Huo ndio mfano wa neno zuri na mti mzuri. Ama mfano wa neno ovu na mti muovu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((وَمَثلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَار))
((Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, uliong'olewa juu ya ardhi. Hauna imara.))
Unaelezea kutokuamini kwa kafiri kuwa ni kama mti usiokuwa madhubuti, mti mchungu kabisa, na bila shaka vitendo vyake havipandi juu wala havitakabaliwi.
Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema kuwa Humthibitisha mwenye kuamini katika maisha ya dunia na pia maisha ya Aakhirah kwa neno hilo lililothibiti kama mti, yaani 'Laa ilaaha illa-Allaah'.
((يُثَبِّتُ اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ وَيُضِلُّ اللّهُ الظَّالِمِينَ وَيَفْعَلُ اللّهُ مَا يَشَاء))
((Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Allaah Hufanya Apendavyo))
Duniani huthibiti kumuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), kwa kuendesha maisha yake yote yakiwa katika mipaka ya Mola wake Mtukufu. Na nje ya maisha ya dunia huthibitika kwa kuweza kujibu maswali atakayoulizwa na Malaika wawili kaburini ambao ni Munkar na Nakiyr:
عَنْ الْبَرَاء بْن عَازِب رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((الْمُسْلِم إِذَا سُئِلَ فِي الْقَبْر شَهِدَ أَنْ لَا إِلَه إِلَّا اللَّه وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُول اللَّه فَذَلِكَ قَوْله (يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ"))) البخاري وَرَوَاهُ مُسْلِم أَيْضًا وَبَقِيَّة الْجَمَاعَة
Imetoka kwa Al-Baraa bin 'Aazib (Radhiya-Llaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu akiulizwa katika kaburi, atashuhudia kwamba: "Laa ilaaha Illa-Allaah wa Anna Muhammadar-Rasuulu-LLaah" (Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mjumbe wa Allaah) hivyo ndiyo maana ya kauli ya Allaah: (Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Aakhirah)) [Al-Bukhaariy, na katika usimulizi mwingine kutoka kwa Muslim na wengineo]
Hadiyth nyingine imeelezea:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ" ((يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاة الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَة)) قَال"(( ذَلِكَ إِذَا قِيلَ لَهُ فِي الْقَبْر مَنْ رَبّك وَمَا دِينك وَمَنْ نَبِيّك ؟ فَيَقُول رَبِّي اللَّه وَدِينِيّ الْإِسْلَام وَنَبِيِّي مُحَمَّد جَاءَنَا بِالْبَيِّنَاتِ مِنْ عِنْد اللَّه فَآمَنْت بِهِ وَصَدَّقْت فَيُقَال لَهُ صَدَقْت عَلَى هَذَا عِشْت وَعَلَيْهِ مُتّ وَعَلَيْهِ تُبْعَث))
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Aakhirah).Akasema: ((Hivyo atakapoulizwa kaburini; Nani Mola wako, nini dini yako, nani Mtume wako? Atasema: Mola wangu ni Allaah, Dini yangu ni Islaam na Mtume wangu ni Muhammad, ametuletea dalili za wazi kutoka kwa Allaah, nikamuamini na nikamsadikisha. Ataambiwa: Umesema ukweli, umeishi kwa hayo, umefia kwa hayo na utafufuliwa kwa hayo)) [At-Twabariy: 16:596]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuthibitishe bil-qawlith-thaabit fil hayaatid-duniya wal-Aakhirah. (Atuthibitishe na kauli thabiti duniani na Aakhirah), Atujaalie tuwe Waumini wa kweli tuweze kufanya vitendo vyema daima vyenye kukubaliwa na Atuwezeshe kujibu maswali tutakayoulizwa kaburin
0 comments:
Post a Comment