WAZIRI wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi amesema miswada iliyowasilishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho haihusu madini pekee, bali pia kulinda rasilimali za kijenetiki na nyinginezo ambazo zimekuwa zikiibiwa kwa muda mrefu.
Akijibu hoja zilizotolewa kwenye Kamati Maalumu ya Pamoja ya Bunge, alisema miswada hiyo inakwenda kulinda maliasili nyingi, ambazo zimekuwa hazipewi nafasi na zina faida kubwa kwa nchini.
“Kwa miaka ijayo, rasilimali za kijenetiki ndizo zitakuwa juu, na kwa bahati mbaya nyingi zimeondoka kabla ya kuwekewa utaratibu, si kuzipoteza pekee, bali pia tumepoteza hata maarifa ya kuzitumia.
Aliongeza: “Ukitaka kujua viti hivi ni vikubwa, ona wanavyovitafuta, nenda Mwenge (Dar) pale akinamama wa Kimasai wanauza dawa, kuna Wazungu wanakwenda kuwahoji namna dawa zao zinatibu, mama yule anaona ufahari, lakini sisi tunadharau maarifa hayo, yanaondoka na tutakuja kuyanunua kwa bei kubwa hapo baadaye.”
Aidha, akijibu hoja ya Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), Kabudi alisema sheria zinazofanyiwa marekebisho zinagusa maliasili ya nchi ambayo iko zaidi ya moja, kwani hawazungumzii madini pekee, pia rasilimali za kijenetiki, masafa, mito, maziwa na mipaka ya bahari kuu.
“Hivyo masuala haya ni mtambuka ambalo linajumuisha wizara nyingi na yanahusu mamlaka ya nchi yaliyojengwa katika misingi wa Katiba, Waziri wa katiba na sheria ndio mwenye mamlaka ya kuyaleta,” alisema.
Awali, Bashe alitaka ufafanuzi wa inakuwaje Waziri wa Katiba na Sheria amepewa mamlaka ya madini wakati utekelezaji wake uko Wizara ya Nishati na Madini. Akijibu swali la Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa (CCM), Kabudi alikiri kuwapo makosa katika muundo na mikataba iliyokuwa ikitumika wakati wa kujadiliana kwenye mikataba na kuwa kuna haja sasa ya kuhakikisha kunakuwa na mikataba badala ya kusubiri mwekezaji kuja na mkataba wake.
“Moja ya matatizo tubadilike na tuje na muundo wetu wa mikataba, kama kuna eneo ambalo tunatakiwa kujipanga vizuri ni kwenye hili na miundo ya mikataba,” alisema. Kabudi alisisitiza kuwa marekebisho ya miswada hiyo, haijalenga kuwafukuza wawekezaji, bali kuhakikisha nchi na wawekezaji wanapata faida katika mikataba hiyo
0 comments:
Post a Comment